Yaliyojiri katika warsha ya wafanyabiashara wa mbao/magogo wa uwanda wa Selous-Ruvuma, tarehe 19 Februari 2016; katika hoteli ya Double M, Lindi mjini

Jumuiko la Maliasili Tanzania (Tanzania Natural Resource Forum-TNRF) pamoja na washirika wake; Shirika la Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo-MCDI, Mtandao wa Jamii wa Usiamizi wa Misitu Tanzania-MJUMITA na Shirika la WWF Tanzania, liliandaa warsha ya siku moja ya wafanyabiashara wa mbao/magogo wa uwanda wa Selous-Ruvuma iliyofanyika siku ya Ijumaa tarehe 19 Februari 2016, Lindi Mjini. Katika uwanda huu wa Selous-Ruvuma, Shirika la WWF Tanzania linafanya kazi na washirika wake (MCDI na MJUMITA) ili kueneza shughuli za Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM).  Warsha hii ya wafanyabiashara iliandaliwa ili kuongeza nguvu katika jitihada hizi kwa kuimarisha mijadala na wafanyabiashara wa mbao/magogo juu ya mambo muhimu yanayosibu biashara ya mazao ya misitu.

Warsha ilikuwa na malengo makubwa mawili: (1) kuwasilisha kwa wafanyabiasha fursa zilizopo za kufanya uvunaji katika misitu ya hifadhi za vijiji (ikilinganishwa na uvunaji katika misitu ya wazi), na (2) kutoa ufafanuzi wa mambo ya kitaalam yahusuyo upimaji na ukadiriaji wa ujazo wa mbao/magogo.

Washiriki wa warsha walikuwa kwenye makundi yafuatayo:

  • Wawakilishi wa wafanyabiashara ya mbao na magogo kutoka uwanda wa Selous-Ruvuma (Kilwa, Liwale, Ruangwa, Rufiji, Nachingwea, Tunduru, Lindi, Masasi)
  • Wawakilishi wa Mamlaka husika za Serikali (Mf. Wakala wa Misitu Tanzania, Idara ya Misitu na Nyuki, TRA)
  • Wawakilishi wa Vijiji vyenye misitu ya hifadhi ((Kilwa, Liwale, Ruangwa, Rufiji, Nachingwea, Tunduru, Lindi, Masasi)
  • Taasisi za Kiraia na Miradi (Jumuiko la Maliasili Tanzania, Kampeni ya Mama Misitu, Shirika la Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo, MJUMITA, WWF Tanzania

MAADHIMIO/MAPENDEKEZO YALIYOADHIMIWA KATIKA KUTATUA CHANGAMOTO MBALIMBALI:

1.Wafanyabiashara kutoshirikishwa katika upangaji wa tozo, bei na uandaaji wa taratibu/mipango mbalimbali inayohusu biashara ya mazao ya misitu

Mapendekezo:

  • Serikali ihakikishe kuwa kuna ushiriki na uwakilishi wa kutosha wa wafanyabiashara ili kufanya tozo, bei na taratibu ama mipango mbalimbali iashirie uhalisia zaidi.
  • Kuunda umoja wa wafanyabiashara wa kanda ya Kusini ili kujenga nguvu ya pamoja kwa wafanyabiashara na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika michakato mbalimbali ya Kiserikali na wadau wengine
  • Umoja wa Wafanyabiashra wa Mbao Lindi (UWAMBALI) kuongoza na kuratibu mchakato wa kuunda mtandao wa pamoja kanda ya kusini

2.Uwepo wa tozo za uvunaji vijijini kinyume na utaratibu (Mfano: Kulipia posho za vikao na michango mbalimbali isitotamkwa kiutaratibu/sheria) na kusababisha wafanyabiashara wengi kukimbilia misitu ya matajiwazi

Mapendekezo:

  • Wafanyabiashara kutolipa zaidi ya posho ya kikao ambayo ni Tshs. 5,000= kwa mjumbe kijijini. Taratibu zingine za vikao zizingatiwe

3.Uwepo wa vituo vingi vya ukaguzi wa mazao ya misitu (utitiri wa vituo) hupoteza muda mwingi, huongeza gharama za usafirishaji na husababisha kujenga mazingira ya rushwa (kwa mfano, kuna vizuizi zaidi ya 19 kati ya Nachingwea na Dar es salaam, na mfanyabiashara anatumia wastani wa dakika 50 katika kila kituo!!)

Mapendekezo:

  • Viwepo vituo vya ukaguzi vya pamoja  na vichache vyenye uwakilishi wa mamlaka mbalimbali za serikali ili kupunguza urasimu usio wa lazima
  • Uwepo wa vituo vichache ama kimoja kwa kila Wilaya
  • Wafanyabiashara kuongeza uaminifu ili kupunguza mianya ya udanganyifu

4.Muda wa usafirishaji kuanzia saa 12 asubuhi mpaka 12 jioni

Mapendekezo:

  • Muda wa usafirishaji uangaliwe tena, na uhesabiwe pale ambapo gari inaingia njia kuu na sio kuanzia maporini.
  • Ni vyema itambulike rasmi kuwa muda wa 12 asubuhi mpaka 12 jioni uwe ni muda wa magari kuwasili vituo vya kukagulia na si muda wa kusafirisha.

5.Usafirishaji katika magari ya wazi

Mapendekezo:

  • Utaratibu uangaliwe upya kwa kuwa usafirishaji katika magari ya wazi (kama inavyopaswa) hupelekea uharibifu wa bidhaa husika hasa pale zinaponyeshewa na mvua. Magari ya wazi na yaliyofungwa (box) yatumike kulingana na uhalisia

6.Kuongezeka kwa uchakataji wa magogo/mbao kwa kutumia CHAINSAW

Mapendekezo:

  • Wafanyabiashara wamekubaliana kwa kauli moja kuacha matumizi ya CHAINSAW na kupendekeza wanaokamatwa na kifaa hicho wapigwe faini kali pamoja na kupelekwa mahakamani
  • TFS iangalie upya utaratibu wao wa kukusanya mapato kwa kuwa umejawa na rushwa zinazopelekea wavunaji/wachakataji kuendelea kutumia CHAINSAW
  • Siku 30 zinazotolewa kwenye kibali cha uvunaji hazitoshi kukamilisha shughuli hiyo kwa kutumia msumeno wa ‘baridi’ hivyo wafanyabiashara wengi kulazimika kutumia CHAINSAW ili kuendana na muda. Ni vyema muda wa kibali uongezwe
  • Ugongaji nyundo magogo na visiki uendane na mahitaji ya wateja na si kwa ratiba ya afisa wa serikali anayehusika ambayo haiendani na muda ambao leseni imetolewa.

7.Kiasi cha ujazo (cubic metre) kinachokatiwa leseni: leseni inatolewa kwa kuanzia cubic metre 20 bila kujali mahitaji ya mfanyabiashara mdogo

Mapendekezo:

  • Leseni itolewe kwa kuzingatia kiwango halisi ambacho mfanyabiashara anahitaji, hata kama ni cubic metre 3 na si lazima 20.

8.Urasimu wa kupata hati ya kusafirishia mazao ya misitu (TP) toka TFS kwa mazao ya misitu yaliyovunwa katika misitu ya hifadhi ya vijiji

Mapendekezo:

  • Warsha imependekeza TP za misitu ya vijiji zitolewe na DFO sababu ndio wenye nyundo ama uangaliwe uwezekano wa kuruhusu vijiji (ambavyo ndio vinatoa leseni) kurushusiwa kutoa pia TP ili kupunguza usumbufu

9.Ushiriki mdogo wa jamii katika usimamizi wa misitu ya Serikali kuu (JFM)

Mapendekezo:

  • Mwongozo wa usimamizi shirikishi wa misitu kwa pamoja (JFM Guidelines) utekelezwe ili wananchi washiriki na wanufaike katika usimamizi wa pamoja. Hii itaongeza motisha na kupunguza uharibifu mkubwa unaoendelea katika misitu ya serikali Kuu

10.Uvunaji katika misitu ya matajiwazi bila uwepo wa mipango ya uvunaji

Mapendekezo:

  • Uvunaji wote ufanyike katika maeno yaliyofanyiwa tathmini na yenye mipango ya uviunaji.

11.Uuzaji wa mbao/magogo kwa kufuata ujazo wa mti mzima uliosimama (standing tree volume)

Mapendekezo:

  • Uuzaji ufanyike kwa ujazo halisi wa magogo au wa mbao na sio mti mzima uliosimama. Upangaji wa bei kwa kuzingatia mti mzima uliosimama unapelekea gharama kuwa juu kwa kuwa upotevu wa sehemu zisizofaa kwa mbao/magogo ni mwingi.
  • Taratibu zinazohusiana na mabaki ya mti (masalia) ziangaliwe upya kwa kuwa zinapelekea wafanyabiashara kukandamizwa na kulipia upya pale ambapo muda wa kuondosha unakuwa umepitiliza, mfanyabiashara hulipia tena upya kama bei ya mti mzima bila kujali haki yake ya awali aliyokwisha kulipia.

12.Sheria haitamki kijiji kinapata nini katika uvunaji wa misitu ya matajiwazi

Mapendekezo:

  • Sheria itamke ni namna gani kijiji kitanufaika katika uvunaji wa misitu ya matajiwazi kwa kuwa TFS ndio yenye mamlaka ya ukusanyaji wa mapato kwenye misitu hiyo

13.Mbao na magogo kugongewa nyundo vijijini kinyume na utaratibu (yaani magogo na mbao vinaondolewa porini na kusogezwa kijijini ili kurahisisha ugongwaji wa nyundo)

Mapendekezo:

  • Utaratibu wa uvunaji ufuatwe na usimamiwe kwa kuwa hali hii inapelekea uharibifu mkubwa na uvunaji holela bila kujali maeneo yaliyofanyiwa tathmini

Warsha hii ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za mradi wa washirika WWF Tanzania na Jumuiko la Maliasili Tanzania unaohusu mambo ya uwekezaji katika misitu na ardhi (unaofadhiliwa na WWF Finland kupitia ofisi za WWF Tanzania) pamoja na shughuli za Kampeni ya Mama Misitu (inayofadhiliwa na Serikali ya Finland). Miradi hii miwili ndiyo itakayogharimia warsha hii.  

Kwa taarifa zaidi, wasiliana na;

Faustine D. Ninga | CBNRM Programmes Coordinator | Tanzania Natural Resource Forum-TNRF | P.O.Box 15605 | Arusha, Tanzania | Mobile: +255 784 252 495 | Email: f.ninga@tnrf.org | Skype: ningafaustine 

Category: 
Location: 
Double M Hotel Lindi , Lindi
Tanzania
Lindi TZ
When: 
19 February 2016 - 4:00pm