UFAFANUZI WA UPOTOSHWAJI KWA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MGOGORO WA ARDHI YA VIJIJI VYA TARAFA ZA SALE NA LOLIONDO

UTANGULIZI

Kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na taarifa za kupotosha kupitia baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo kipindi Maalum kilichoitwa Loliondo Special kilichorushwa Channel Ten tarehe 10 Januari 2015 na kurudiwa tarehe 17 na pia kupitia makala iliyochapishwa kwenye gazeti Gazeti la Jamhuri toleo namba 171 la tarehe 13-19 Januari 2015 yenye kichwa cha habari, “Shirika hili ni hatari kwa usalama wa Taifa” na gazeti la Jamhuri la tarehe 18-24 November 2014 toleo namba 163 lenye kichwa cha habari “Wakenya, NGOS wanavyoivuruga Loliondo”.

Sisi Asasi za Kiraia kwa ujumla wetu baada ya kuchambua na kufuatilia upotashaji huu tuna mambo haya ya kusema: Kwanza tunalaani vitisho na propaganda zote chafu zinazofanywa na OBC, Wizara ya Maliasili na Mbunge wa Ngorongoro dhidi ya ASASI za Kiraia na watetezi wote wa ardhi ya wafugaji loliondo, Pili tunapenda kutoa ufafanuzi wa upotoshaji mkubwa unaofanywa na makundi hayojuu ya mgogoro wa ardhi wa Loliondo, Tatu tunaitaka OBC pamoja na Mbunge kuacha kutumia nguvu nyingi na pesa kuigawa jamii ya Ngorongoro kwa lengo la kutaka kupokonya ardhi yao.

(A)   KUHUSU ASASI ZA KIRAIA NA WATETEZI WA ARDHI YA WAFUGAJI

Ni ukweli usiopingika kuwa bila utetezi wa AZAKI katika migogoro mbalimbali ya ardhi hapa nchini hasa huu wa Loliondo, ni dhahiri ardhi ile ya Loliondo isingekuwa mikononi wa wafugaji hivi leo. Katika harakati zote za kuwapokonya wananchi ardhi hii, asasi za kiraia au kwa dhamana yake zenyewe ama kwa kuombwa na wananchi wa maeneo husika zimekuwa zikifuatilia na kutoa taarifa juu ya ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu zinazofanywa dhidi ya wananchi wa Loliondo tangu mgogoro huu ulipoanza mwaka 1992. Asasi hizi sio za Loliondo pekee bali ni asasi kutoka nchi nzima ya Tanzania na hata nje ya Tanzania ambazo zina dhamana ya kulinda na kutetea haki za binadamu.

Kutokana na kutambua umuhimu wa watetezi hawa kutaka kuelimisha jamii juu ya haki zao na kuzuia uporaji wa ardhi hiyo, wahusika sasa wamekuja na njia zifuatazo ili kudhoofisha kazi za watetezi wa jamii;

(i)   Kutumia kete ya Uraia kutishia watetezi binafsi na mshirika

Kumekuwepo na harakati za kupotosha ukweli juu ya uraia wa wananchi wanaoishi Loliondo ambao serikali imekuwa na mpango wa muda mrefu wa kuwaondoa. Mkakati huu ulianza mwaka 2009 wakati wa uchomaji wa makazi ya wananchi kwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii wakati waandishi wa habari pamoja na watetezi wengine waliokuwa mstari wa mbele kufichua vitendo vya uvunjifu wa haki ya ardhi huko loliondo ulipofanyika.

Wafugaji na watetezi wao wamekuwa wakipokea vitisho hadi kufikia wakati wengine wamekuwa wakituhumiwa kuwa sio watanzania bali ni Wakenya. Vitisho hivyo ni sehemu ya njia ya kuzinyamazisha AZAKI pamoja na watetezi wa haki za jamii kwa lengo la kuupotosha umma na kufanya waache kufuatilia suala hili. Pia tujiulize kwani nini suala hili la urai linazungumzwa tu kwenye hoja hii ya mgogoro wa OBC.

Vitisho kwa watetezi wa haki za wafugaji wakiwemo waandishi wa habari, havijashuhudiwa Loliondo tu bali hata maeneo mengine ya nchi ambayo yana idadi kubwa ya wafugaji kama vile Kiteto, Hanang, Kilosa, Morogoro, Mbeya, Mara, na Rukwa na sababu mojawapo ya vitisho

hivyo ni kutaka wafugaji waachie maeneo yao kwa ajili ya wawekezaji walio katika maeneo hayo.

(ii)   Kutoa maelezo hasi  na potofu juu ya fedha zinatolewa kwa ajili ya kuendesha AZAKI na kufanya kazi za utetezi

Sisi asasi za Kiraia, tumesikitishwa sana na nguvu kubwa iliyotumika OBC na wafuasi wake kupitia mtengenezaji wa kipindi kilichorushwa na TV ya Channel Ten, Jerry Muro, yenye kulenga kwa makusudi kuzichafua kazi zinazofanywa na asasi za kiraia na kuwashambulia baadhi ya watetezi wa ardhi ya wananchi. Taarifa hizi za upande mmoja zinatia shaka dhamira nzima ya kuandaa kipindi, uweledi na umakini wa mwandaaji lakini pia zinaitia doa tasnia ya habari nchini kuwa inaweza kutumiwa kwa namna yoyote na mtu yoyote mwenye fedha zake kuupotosha umma kwa maslahi yake.

Kwa mtu yeyote anayejua ukweli wa mgogoro wa Loliondo, anashawishika kuamini fedha nyingi zinatumika kununua baadhi vyombo vya habari na wanahabari wasiokuwa na maadili ili kupoteza ukweli ikiwa ni katika harakati za kuendelea kupora ardhi ya Loliondo. Tunasikitika pia kuona kwamba waandishi hawa wachache wanasahau jinsi ambavyo serikali mwaka 2009 iliwasingizia wanahabari wa Chanel Ten na gazeti la mwanachi kwamba ndio waliochoma maboma na kupiga picha moto ukiwaka kwa lengo la kupotosha habari

(iii)   Kurubuni baadhi ya waandishi, baadhi ya viongozi wa mila na AZAKI mojawapo kwa lengo la kugawa jamii na kuzichafua ASASI zinazotetea na kutoa elimu kwa jamii na kuisafisha OBC

Ili kupotosha ukweli na jitihada za watetezi wa haki za binadamu kumekuwepo na mkakati wa kuonyesha wananchi kufaidika kwa njia mbalimbali na uwepo wa makampuni ya kigeni hususan OBC ambao umekuwa ukitumiwa na baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wa habari wenye uchu wa fedha, na kuwarubuni baadhi ya viongozi wa jamii ili kutoa taarifa za upotoshaji wa kile wanachokiita “ukweli kuhusu mgogoro wa Loliondo” Waandishi hawa wa habari, Jerry Muro na Manyerere Jackton wa Gazeti la Jamhuri wamekuwa wakitumiwa na OBC kwenda kuwahoji wafuasi wa OBC kule Lolindo na kudai kuwa ndio maoni ya wananchi. (Rejea Makala za Gazeti la Jamhuri na ya Jerry Muro Kupitia Chanel Ten kuhusu Loliondo).

Habari hizo si za kweli na zina lengo la kuhadaa umma kwamba OBC ni kampuni inayokubalika kijamii na ambayo inaleta maendeleo kwa jamii. Sambamba na kuisafisha OBC, waandishi hawa wamekuwa wakitumika kuzichafua AZAKI na kuonyesha kwamba ndio chanzo cha mgogoro huku wakijua kwamba OBC kupewa ardhi hiyo ndio chanzo cha mgogoro.

(B)   UKWELI KUHUSU MGOGORO WA ARDHI LOLIONDO

Kama tulivyoeleza katika tamko letu kwa vyombo vya habari la tarehe 22/4/2013 tunasisitiza kusema kwamba eneo la Loliondo ni eneo la vijiji ambavyo vinatambulika kisheria tangu wakati wa ukoloni na kulindwa kisheria na sheria ya ardhi ya vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na sheria ya Serikali za Mitaa, Tawala za Wilaya namba 7 ya Mwaka 1982. Eneo hili pia limekuwa likijulikana kama pori tengefu la Loliondo kulingana na sheria ya wanyama pori ya mwaka 1974 na sheria ya wanyama pori namba 5 ya mwaka 2009 ambazo zote hazija badilisha hadhi ya vijiji vilivyopo wala haki za ardhi za wenyeji wa vijiji husika wala hazihamishi haki hizo kwenda kwa mamlaka nyingine yoyote ikiwemo wizara ya malisaili na Utalii au kampuni ya OBC.

Itambulike  kwamba  hadhi  ya  pori  tengefu  haingilii  hadhi  ya  umiliki  wa  ardhi  bali  inatoa mamlaka kwa mkurugenzi wa wanyama pori kusimamia wanyama pori waliopo katika eneo hilo pamoja na kutoa mamlaka ya kugawa vitalu vya uwindaji kwa makampuni ya uwindaji bila kuingilia haki za ardhi kwa wakazi wa maeneo husika. Huu ndio ukweli juu ya hadhi ya kisheria ya ardhi ya Loliondo na kinachodaiwa na vyombo vya habari kuwa ndio ukweli ni upotoshwaji mtupu.

 

Tunazidi kusisitiza kwamba mgogoro wa Loliondo unatokana na serikali kutaka kupokonya ardhi ya vijiji bila ridhaa ya wananchi na wala kufuata utaratibu kisheria ili kutanua wigo wa kibiashara wa wawekezaji ambao wanaendesha biashara ya uwindaji wanyamapori.

Kama tulivyoeleza katika matamko mbalimbali katika miaka ya nyuma,  tunaendelea kutoa ufafanuzi wetu juu ya upotoshaji huu kama ifuatavyo:

  • Ardhi inayopiganiwa kumegwa na serikali kwa manufaa ya wawekezaji binafsi ni mali ya vijiji vya Loliondo ambavyo vimekuwa vikitumia eneo hilo kwa ajili ya malisho ya mifugo yao tangu kabla ya Ukoloni. Juhudi zozote za kutaka kuimega kwa kutumia propaganda za uchochezi wa baadhi ya vyombo vya habari kupotosha ukweli ni ukiukwaji mkubwa wa haki za wananchi wa Tanzania, hasa wakazi wa Loliondo, na ni kinyume kabisa na maadili ya tasnia ya uandishi wa habari.
  • Hoja kuwa tokea enzi za ukoloni eneo la Loliondo lilikuwa ‘eneo la serikali na si la wananchi’ si kweli, kwa msingi kwamba hata kama eneo la Loliondo lilifanywa kuwa pori tengefu, bado sheria inatambua eneo hilo kuwa ni ardhi ya vijiji na ndio sababu sheria hizi lazima ziheshimiwe na kuzingatiwa kila mara suala la ardhi ya vijiji linapoguswa.
  • Hoja ya upotoshaji kwamba Pori Tengefu la Loliondo lilitengwa mwaka 1974 kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori peke yake si kweli kama ilivyorushwa katika kipindi maalum cha television ya Channel Ten. Ukweli ni kuwa kabla ya eneo husika kutangazwa kuwa eneo la pori tengefu, tayari kulikuwepo watanzania wengi waliokuwa wanaishi hapo kwa wingi wakifanya shughuli za kilimo na ufugaji, na  wala hawakupoteza uhalali wao wa kusihi maeneo hayo wakati wa kuanzishwa kwa pori tengefu la Loliondo na hata baada ya hapo. Na ikumbukwe kuwa wananchi wa Loliondo walio wengi walikuwa wanaishi Loliondo na wameendelea kuwa hapo na hata wangetaka kutawanyika zaidi isingewezekana maana walikatazwa kuishi Serengeti na wakoloni wa kizungu mwaka 1959 na wengine wao waliokuwa wanaishi ndani ya Serengeti kulazimishwa kubaki Loliondo baada ya uundwaji wa Serengeti National Park.
  • Hoja ya kwamba watu katika vijiji vya Loliondo wameongezeka zaidi kutokana na ujio wa wahamiaji wa Kikenya haina mashiko na ni mojawapo tu ya mbinu ya kuwaondoa wananchi wa Loliondo kwa visingizio mbalimbali kama ilivyojitokeza mwaka 2009 wakati wa uchomaji wa maboma na ukiukwajji mkubwa wa haki za binadamu. Ndiyo maana hoja ya kuwa ni Wakenya ni ya upotoshaji mkubwa ili kujipatia uhalali wa kuwavunjia wananchi makazi yao kwa maslahi ya mwekezaji. Hoja hii ilitumika na aliyekuwa Waziri wa maliasili na Utalii Shamsa Mwangunga kuidhinisha operesheni ya kuchoma makazi ya watu Loliondo mwaka 2009 na kusababisha ukiukwaji wa haki za binadamu kwa watanzania hao. Ikumbukwe kuwa, katika operesheni hiyo hakukuwa na Mkenya yeyote aliyechomewa nyumba bali wote walikuwa ni Watanzania.
  • Tunasikitika kwamba sababu hiyohiyo leo inatumika tena kuhadaa ulimwengu uamini kuwa wanaoondolewa Loliondo si wenyeji bali ni Wakenya. Na hata kama wangekuwa ni Wakenya basi serikali inaonyesha udhaifu mkubwa wa kuachia wageni kuingia nchini na kujistawisha kiasi cha kuweka makazi na kuendesha maisha yao bila kuingiliwa kwa muda wote huu wa miaka ziadi ya 20. Aidha, hata kama wangekuwa wakenya, basi serikali ingetumia taratibu za kimataifa katika kushughulikia wahamiaji haramu badala ya kuchoma makazi ya raia wake kwa kisingizio cha wakenya. Wanadai 70% ya wakazi wa Lolindo ni Wakenya, hoja hii ni aibu kwa Taifa. Loliondo ni eneo la wafugaji wa kimaasai hata kabla ya kuja kwa wakoloni, hivyo iweje leo wabaguliwe na kukanwa uraia wao kwa sababu tu ya kujali maslahi ya wawekezaji wa kigeni?
  • Tunasikitika pia kuiona OBC ikitamba kupitia vipindi Maalum vya televisheni ya chanel Ten kuwa ndio ilyotekeleza miradi mbalimbali kwa wananchi wa Loliondo huku wakijua wazi kuwa baadhi ya miradi hiyo imetekelezwa na Ubalozi wa Umoja wa Falme Kiarabu na Water Aid, Mradi wa afya wa Hospitali ya Wasso na Kanisa Katoliki Jimbo la Arusha, pamoja na miradi mingine mbalimbali iliyotekelezwa na asas iza kiraia kwa kushirikiana na wananchi.
  • Tumesikitishwa pia na taarifa za Mbunge wa Ngorongoro ambaye ni naibu waziri wa Mifugo, Ndugu Kaika Telele, ambaye pia amefanya kazi kwa ushirikiano na asasi za kiraia kwa miaka yote ya utetezi wa ardhi ya Loliondo kugeuka ghafla na kuitetea kampuni ya OBC.  Haya mapenzi ya dharura kati yake na OBC yametokea wapi?

Kutokana  na  matukio  hayo  ya  hivi  karibuni,   sisi  Mashirika  yasiyo  ya  kiserikali tunatoa matamko yetu   na kuendelea kusisitiza kama ifuatavyo:

Serikali na washirika wake hasa makampuni ya uwindaji waache mara moja kupotosha umma kwamba ardhi hiyo siyo ya vijiji na wazingatie sheria kwa kuvipa vijiji haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe kwa kutumia sheria zilizopo za ardhi na za serikali za mitaa.

Kampuni ya OBC na wafuasi wake waache mara moja visingizio kwamba mgogoro wa Loliondo unasababishwa na wanaharakati na mashirika ya nje kwani yenyewe inatambua uwepo wa mgogoro huo unasababishwa na maamuzi ya serikali ya kugawa ardhi ya wananchi bila kuwashirikisha kwa kuangalia upande mmoja wa manufaa kwa wawekezaji tu bila kuangalia athari kwa wananchi.

Serikali iheshimu na kusimamia sheria za ardhi hususan sheria ya ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 inayotambua uhalali wa ardhi za vijiji na kuvipa mamlaka vyombo vya ngazi hiyo kusimamia ardhi hiyo.

Tunataka mkakati wa kupotosha ukweli na kurubuni waandishi na vyombo vya habari ili kuendeleza harakati za kujitwalia ardhi ya wananchi usitishwe na wale wote wanaohusika na mkakati huo. Halikadhalika OBC iache kutumia pesa kugawa wananchi kwa maslahi binafsi.

Tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na vyombo vya habari kuelimisha umma, ila tunavisihi na kuvitahadharisha viwe makini na baadhi ya waandishi wa habari, wanaokosa weledi kwenye kazi zao, na kuhakikisha kwamba kila habari inayofika mezani kwao inahambuliwa kwa umakini ili kuhakikisha waandishi wanaotumia tasnia hii kinyume na maadili mazuri ya vyombo vya habari wanachukuliwa hatua za kinidhamu. Pia tunaliomba Baraza la Habari Tanzania liendelee kuwafuatilia wale wote wanaokiuka maadili ya uandishi, ili kurejesha heshima ya kazi hii na hatimaye kuliletea taifa maendeleo kwa haki na usawa.

MWISHO

 

Pamoja na kuwepo kwa taarifa hizi na zile zote zinazofanania hizi, asasi za kiraia hatutoacha kupigania haki za wanyonge na wale ambao sauti zao zinaminywa kwa nguvu ya dola au wenye nguvu za kiuchumi. Tunajua gharama ya wito huu ni kubwa lakini kwa takribani miaka 23 ya mageuzi nchini tumeamua kubeba jukumu hili zito na kubwa licha ya changamoto nyingi za kutishiwa, kukamatwa, kuhojiwa mara kwa mara na kazi zetu kuchunguzwa na kuingiliwa. tunaheshimu sana mchango wa vyombo vya habari katika utetezi na tusingetarajia kuona waandishi wa habari wa nchi hii wanakuwa sehemu ya matukio ya kujeruhiwa kwa wanaharakati, ama kufungiwa kwa mashirika yanayotetea haki za binadamu ukanda wa Loliondo, kwakuwa nafasi ya waandishi kuleta mabadiliko ni kubwa mno kuliko kudidimiza sauti za wanyonge. Pia tutasikitika kama tasnia ya habari itakubali kuwa sehemu ya makundi yanayotaka kufanikisha ardhi ya wafugaji wanyonge huko Loliondo iende mikononi wa matajiri wanaojinufaisha kwa mal iza watanzania bila huruma. Si vema kabisa kwa wana habari kujiingiza katika propaganda chafu hasa wakati huu nchi yetu inapoingia katika matukio makubwa ya kuamua mustkabali wa maendeleo ya taifa letu kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Kufanya hivyo kutawachonganisha waandishi wa habari na wananchi badala ya kuwa kiungo kati yao na wadau wengine muhimu wa maendeleo ya taifa letu.

Imetolewa leo tarehe 22 Januari 2015 na Mashirika yafuatayo.

TAMKO HILI LIMETOLEWA LEO TAREHE 22 January 2015 NA MASHIRIKA AMBAYO NI;

  1. PINGOs Forum
  2. Tanzania Land Alliance- TALA
  3. HAKIARDHI
  4. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu- LHRC
  5. Tanzania Human Rights Defenders Coalition
  6. Ujamaa Community Resource Team- CRT
  7. Pastoralists Women Council –PWC
  8. Ngorongoro NGOs Network –NGONET
  9. Tanzania Pastoralists Community Forum-TPCF
  10. Indigenous Heartland Organization
  11. TANLAP
  12. SHARINGO
  13. TNRF
Undefined